RAIS MAGUFULI AWAPA ONYO WAFANYABIASHARA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amewaonya wafanyabiashara wanaopandisha bei za vyakula katika msimu huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Rais Magufuli ametoa rai hiyo leo wakati akihutubia maelfu ya Watanzania waliofika katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam kushuhudia mashindano maalumu ya 20 ya kusoma Qur'aan tukufu barani Afrika, yanayoandaliwa na taasisi ya AL-hikma ya nchini Tanzania.
Magufuli amesema kuwa kitendo cha kupandisha bidhaa hizo hakimpendezi mwenyezi Mungu kwani mfanyabiashara hawezi kutajirika kwa kipindi cha mwezi mmoja, bali ni kujichumia dhambi.
“Natoa wito wa wafanyabiashara kuacha kupandisha bei za bidhaa ambazo zinatumiwa na ndugu zetu Waislamu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan, mamlaka za serikali zifuatilie suala hili kwa karibu”, amesema Rais Magufuli.
Ameongeza kuwa, "kufunga katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan au Kwaresma bila ya kuyaishi maneno yaliyo kwenye vitabu vitakatifu ni kazi bure, sote kwa pamoja tuungane kuwasindikiza wenzetu kukamilisha mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan".
Kilele cha mashindano hayo kimehitimshwa kwa kutangazwa washindi watano kati ya 20 ambao walishindana kutoka mataifa kadhaa barani Afrika. Mshindi wa kwanza ni Mohamed Diallo (23) wa Senegal ambaye amejishindia zawadi ya Sh. 20 milioni pamoja na tiketi ya kwenda kuhudhuria ibada ya Hijjah nchini Saudi Arabia.
Comments
Post a Comment