KANGI LUGOLA AGEUKIA MAKANISA NA MISIKITI
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema kuna baadhi ya watu ambao wanajipenyeza kupitia mgongo wa taasisi za dini kujifanya wahubiri kumbe ni wachochezi na wanajiingiza katika masuala ya kisiasa.
Amesema wizara yake iko makini katika kusajili makanisa na misikiti yote nchini na kwamba mpaka sasa imepokea maombi mengi ambayo yametumwa kuomba usajili.
Lugola aliyasema hayo jana wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Sunsi, Kata ya Nampindi, Mwibara, Bunda mkoani Mara.
Alisema baadhi yao waombaji hawajapata usajili kwa sababu wanahitaji umakini mkubwa katika kufanya uchunguzi wa kina kabla hawajatoa usajili na kwamba lengo ni kuepusha baadhi ya taasisi za dini zenye mpango mbaya na maendeleo ya nchi.
Lugola ambaye ni Mbunge wa Mwibara, alisema taasisi za dini zina mchango mkubwa nchini na uwapo wao ni muhimu katika maendeleo ya nchi na serikali inauthamini mchango wao katika kuimarisha amani na kuwaweka watu pamoja.
Alisema pamoja na kulitambua hilo, baadhi ya dini hizo zinakiuka utaratibu wa usajili na kuvunja sheria za nchi kwa kuacha kuhubiri masuala ya kiroho na badala yake kujihusisha na masuala ya kisiasa na uchochezi.
“Serikali ya awamu ya tano haitakuwa tayari kwa mwananchi yeyote kutumia mwavuli wa dini au kufanya misikiti na makanisa kuwa kichaka cha kufanya uchochezi na kuhatarisha amani ya nchi hii. Tuko makini na hatuwezi kuchezewa na mtu yeyote au taasisi yoyote,” alisema Lugola.
Lugola alitumia muda mrefu kutoa ufafanuzi huo baada ya kukaribisha maswali mbalimbali kutoka kwa wakazi wa kijiji hicho katika mkutano huo ili wananchi hao waweze kuuliza ndipo mmoja wao akauliza kuhusu uchelewashaji wa usajili wa kanisa.
“Taasisi hizi za makanisa na misikiti wanao mchango mkubwa sana kwa wananchi hususani waumini wao katika kuhubiri amani ya nchi hii, katika kukemea vitendo vya rushwa kwasababu hata katika maandiko rushwa imekemewa, rushwa imeonekana ni hatari katika vitabu vyote vitakatifu vya dini,” alisema
“Wako baadhi ya watu wasiowaaminifu nchini wamejipenyeza na wanaendelea kujipenyeza katika taasisi hizo na badala ya kuhubiri masuala ya kiroho, wanajihusisha na masuala ya uchochezi na uvunjifu wa amani,” alisema Lugola.
Lugola alisema serikali haitakubali kuchezewa na kutokana na sababu hizo na nyinginezo, Wizara yake inaendelea kuwa makini kuyafanyia kazi maombi ya taasisi hizo kwa kuomba usajili na aliwataka ambao wametuma maombi yao kwa muda mrefu waendelee kusubiri wakati serikali ikiendelea kuwa makini kuyafanyia kazi maombi yao.
Pia Lugola aliwataka wananchi nchini waendelee kutoa taarifa za uhalifu, majambazi na vibaka ili Jeshi la Polisi lifanye kazi na waone makali ya jeshi hilo katika utendaji wa kazi kwa sababu askari waliapa kulinda usalama wa raia na mali zao.
Waziri huyo aliwataka Watanzania waendelee kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu kwa kuwa jeshi la polisi liko imara na linafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani.
Comments
Post a Comment