KLABU YA SIMBA YAANZA MAZOEZI NCHINI ZAMBIA
Klabu ya soka ya Simba imeeleza kupokelewa vizuri na viongozi wa klabu ya soka ya Power Dynamos ya Zambia chini ya Rais wao pamoja na CEO wa timu, ambao pia wamewapatia uwanja wa kufanyia mazoezi.
Viongozi hao wa Power Dynamos walikutana na viongozi wa klabu ya Simba akiwemo mtendaji mkuu Crescentius Magori, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Dkt. Zawadi Kadunda, pamoja na Msemaji Haji Manara na kuzungumza mengi.
Pamoja na mambo mbalimbali ya kiutendaji waliyoongea viongozi hao, msemaji wa Simba Haji Manara amesema viongozi wamemwambia umaarufu wa mchezaji Clatous Chama umeongezeka maradufu nchini humo kutokana na video zinazomwonesha akifanya matukio muhimu uwanjani akiwa na Simba ikiwemo kufunga na kutengeneza mabao.
Umaarufu wa Chama haujawa mkubwa nchini Zambia pekee bali hata hapa nchini Tanzania, ambapo mashabiki wengi wamekuwa wakimfananisha na kiungo wa klabu hiyo, Mrwanda, Haruna Niyonzima kwa staili ya kiuchezaji. Chama ana mabao matatu mpaka sasa kwenye kampeni ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
Simba inafanya maandalizi ya mwisho ya mchezo wake wa klabu bingwa Afrika dhidi ya Nkana Red Devils ambao utapigwa Jumamosi Desemba 15, 2018 mjini Kitwe Zambia.
Comments
Post a Comment