KUKOSA KITAMBULISHO CHA TAIFA NI KOSA KISHERIA - WAZIRI KANGI LUGOLA
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka wananchi wenye sifa ya kupata Vitambulisho vya Taifa nchini waende kujisajili katika ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho hivyo (NIDA) zilizopo katika Wilaya wanazoishi kwakuwa ni lazima kila Mtanzania awe nacho.
Akizungumza na wananchi wa Mji wa Kibara, Jimbo la Mwibara, Bunda, Mkoani Mara, Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo, alisisitiza kuwa ni lazima kila mwananchi raia wa Tanzania awe na kitambulisho cha Taifa.
“Vitambulisho hivi ni muhimu kuwa navyo, nawaomba Watanzania msipuuze hili zoezi, na pia napenda kusisitiza kwa mara nyingine muelewe vizuri kuwa vitambulisho hivyo vitatolewa kwa watanzania wenye sifa tu ambao watapita katika mchujo ili kuepusha kutoa kwa wasio raia,” alisema Lugola.
Aidha Lugola alisema wapo wananchi ambao hawakujitokeza wakati usajili ulipokua unafanyika katika mitaa na vijiji vyao, na pia wapo ambao kipindi hicho walikua na miaka 17 na kukosa sifa ya kujisali, lakini kwasasa wamefikisha miaka 18, nao wanapaswa kufika ofisi za wilaya ili wapate huduma hiyo ya usajili.
Lugola aliongeza kuwa, NIDA ipo makini na pia watahakikisha kuwa wanasajili wananchi nchi nzima kwa umakini na pia kutoa elimu zaidi kuhusiana na kuwa na kitambulisho hicho kwasababu kuna baadhi ya watanzani bado hawajajua umuhimu wa kuwa na kitambulisho cha taifa.
www.bongotrending1.blogspot.com
Comments
Post a Comment